Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) limefanikiwa kuratibu na kuendesha Kikao cha Pamoja cha Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Majukwaa ya Ushirika ya Mikoa Tanzania Bara kilichofanyika tarehe 01 Oktoba, 2026 katika Ukumbi wa Rafiki Hotel, Jijini Dodoma.
Kikao hiki kiliwakutanisha viongozi hao pamoja na Waratibu na Wawakilishi kutoka TFC, TCDC, MoCU, na COASCO.
Katika ufunguzi wa kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TFC Ndg. Fares Muganda alisisitiza kuwa Majukwaa ya Ushirika ya Mikoa yalianzishwa kama nyenzo na daraja muhimu la kuimarisha ushirikiano, mawasiliano, uratibu na ushirikishwaji wa wadau wote wa sekta ya ushirika katika ngazi ya mkoa. Aliongeza kuwa mafanikio ya majukwaa haya yatategemea ushiriki wa dhati, uwazi katika kutoa maoni, na utayari wa kujifunza kutoka kwa uzoefu wa mikoa mingine ili kuongeza mchango wa ushirika katika ujenzi wa uchumi jumuishi, shindani na endelevu.
Mambo Makuu Yaliyojadiliwa na Kutathminiwa:
• Tathmini ya Utekelezaji: Kuangalia kwa kina utekelezaji wa shughuli na mafanikio ya majukwaa tangu kuanzishwa kwake.
• Boresho la Mwongozo: Kupokea maoni ya maboresho ya Mwongozo wa Usimamizi na Uendeshaji wa Majukwaa ya Ushirika ya Mikoa.
• Ushirikiano na Mikakati: Kujadili wajibu wa kila mdau, uendelevu, ushirikishwaji wa wadau, na uendeshaji wa Jukwaa la Wanawake wa Ushirika.
• Uelekeo wa Mbele: Kuweka msingi mzuri na kuandaa kalenda ya kazi ya majukwaa kwa mwaka 2027 na miaka ijayo.
TFC inaahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha majukwaa haya yanakuwa chombo madhubuti cha maendeleo ya ushirika nchini!
"Pamoja Tujenge Uchumi"