Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesisitiza dhamira ya Wizara ya kuendeleza tasnia ya mazao ya bustani ili kuongeza mchango wake katika pato la taifa na mapato ya fedha za kigeni, kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, leo amefungua rasmi Maonesho ya Kimataifa ya Bidhaa na Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, katika Viwanja vya TGT, Arusha.
Katika hotuba yake, Makamu wa Rais ameeleza kuwa Serikali inaendelea na taratibu za kufungua masoko mapya ya mazao ya bustani, sambamba na kuwajengea wakulima uwezo wa kukidhi viwango vya kimataifa. Pia ameielekeza TanTrade kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo TAHA kubaini bidhaa zinazohitajika katika masoko hayo na viwango vya ubora vinavyotakiwa ili kuwaongoza wazalishaji.
Akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesisitiza dhamira ya Wizara ya kuendeleza tasnia ya mazao ya bustani ili kuongeza mchango wake katika pato la taifa na mapato ya fedha za kigeni, kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Kwa vyama vya ushirika, fursa hii inaweka umuhimu wa kuratibu uzalishaji kwa kuzingatia mahitaji ya soko, kukusanya mazao kwa pamoja na kuhakikisha ubora na upatikanaji wa bidhaa kwa wakati.
Kupitia Banda la Ushirika, Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) linatumia maonesho haya kutangaza bidhaa za vyama, kuviunganisha na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi, wasafirishaji, wawekezaji na watoa huduma katika mnyororo wa thamani.
Mazungumzo ya kibiashara yanayoratibiwa na TFC yanatoa nafasi kwa vyama kufahamu aina, kiasi na viwango vya ubora wa mazao yanayohitajika sokoni, kujadili mifumo ya kilimo cha mkataba na mikataba ya ugavi, pamoja na kutafuta ushirikiano katika uhifadhi, ufungashaji, usindikaji na uongezaji thamani.
Mwelekeo wa TFC ni kusaidia vyama vya ushirika kutoka katika uzalishaji usiozingatia mahitaji mahsusi ya soko na kuelekea biashara yenye mipango ya uzalishaji, ubora unaotambulika na mahusiano ya moja kwa moja na wanunuzi.
HortiLogistica Africa 2026 ni fursa ya kuendeleza mahusiano hayo na kuweka msingi wa mikataba na uwekezaji wenye manufaa kwa vyama vya ushirika na wanachama wake.