KOROSHO BORA, MALIPO KWA WAKATI: WADAU WAJIPANGA KUIMARISHA MSIMU WA MAUZO

By TFC Super Admin

Kikao kimewakutanisha viongozi na watendaji wa Vyama Vikuu kutoka MAMCU na TANECU, TFC, wawakilishi wa Benki Kuu ya Tanzania Kanda ya Kusini, CoopBank, NMB Bank, TCB, CRDB Bank, Exim Bank, NBC Bank na Azania Bank, pamoja na kampuni za mawasiliano na huduma za fedha ikiwemo Mixx by Yas, Vodacom na Airtel.

KOROSHO BORA, MALIPO KWA WAKATI: WADAU WAJIPANGA KUIMARISHA MSIMU WA MAUZO
KOROSHO BORA, MALIPO KWA WAKATI: WADAU WAJIPANGA KUIMARISHA MSIMU WA MAUZO
Juhudi za kuhakikisha msimu wa mauzo ya korosho 2026/2027 unaendelea kwa ufanisi, uwazi na kuzingatia maslahi ya wakulima zimepata msukumo zaidi mkoani Mtwara, baada ya wadau wa sekta ya fedha, mawasiliano na ushirika kukutana kufanya tathmini na kuweka mikakati ya kuboresha malipo ya fedha za mauzo ya korosho kwa wakulima.

Kikao hicho, kilichoitishwa na kuratibiwa na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara, Bw. Robert Nsuza, ni mwendelezo wa juhudi zinazofanywa na Ofisi ya Mrajisi, Vyama Vikuu vya Ushirika, Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Bodi ya Korosho Tanzania, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Serikali za Mkoa na Wilaya pamoja na wadau wengine kuhakikisha korosho bora zinazozalishwa nchini zinakusanywa, kuhifadhiwa na kuuzwa kupitia mifumo rasmi huku ikiwa na ubora wa hali ya juu.

Kikao kimewakutanisha viongozi na watendaji wa Vyama Vikuu kutoka MAMCU na TANECU, TFC, wawakilishi wa Benki Kuu ya Tanzania Kanda ya Kusini, CoopBank, NMB Bank, TCB, CRDB Bank, Exim Bank, NBC Bank na Azania Bank, pamoja na kampuni za mawasiliano na huduma za fedha ikiwemo Mixx by Yas, Vodacom na Airtel.

Msisitizo wa Malipo kwa wakati na kupunguza miamala inayokataliwa

Sehemu kubwa ya majadiliano iilijikita katika kutathmini mwenendo wa malipo ya fedha za mauzo ya korosho na changamoto za miamala inayorejeshwa bila kukamilika kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo akaunti zisizotumika kwa muda mrefu, tofauti za majina ya wakulima na taarifa zisizo sahihi za namba za akaunti.

Wadau hao wa fedha wamekubaliana kuimarisha usajili na uhakiki wa taarifa za wakulima, kuboresha mawasiliano kati ya benki na Vyama Vikuu, kufuatilia miamala inayokwama na kuhakikisha changamoto zinapatiwa ufumbuzi mapema ili wakulima wapokee malipo yao ndani ya muda.

Aidha, msisitizo uliwekwa tena kwa taasisi za fedha na watoa huduma za malipo kuendelea kushirikiana na vyama katika kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya akaunti, umuhimu wa taarifa sahihi na taratibu za kupokea malipo ya mazao.

Akichangia katika kikao hicho, Mwenyekiti wa MAMCU, Bw. Alhaji Jula Jula, amesisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na ushirikiano wa karibu kati ya wadau wote. Amehimiza maslahi ya wazalishaji, hususan wakulima wadogo, kupewa kipaumbele na kuhakikisha malipo yao hayacheleweshwi.

Wadau wahamasishwa kuchangia vifaa dhidi ya athari za mvua

Katika hatua nyingine, TFC imehimiza kuimarishwa kwa elimu na utoaji wa taarifa sahihi kuhusu msimu wa korosho, ikiwemo njia bora za ukusanyaji, ukaushaji, uhifadhi na usimamizi wa ubora wa mazao.

Mwakilishi wa TFC, Bw. Juma Bruno, ametoa wito kwa taasisi za fedha, kampuni za mawasiliano na wadau wengine kushirikiana katika upatikanaji wa vifaa na rasilimali za kuboresha mazingira ya ukaushaji na uhifadhi wa korosho, hususan maturubai, ikiwa ni hatua ya kujiandaa na kupunguza hatari za mvua zinazotarajiwa katika mikoa ya Kusini.

Wadau wameonesha nia ya kuunga mkono jitihada hizo, huku wakikubaliana kuendeleza ushirikiano kupitia utaratibu rasmi wa kubainisha mahitaji, kupokea ahadi na kuratibu michango. TFC itashirikiana na Vyama Vikuu na Ofisi ya Mrajisi kuhakikisha rasilimali zitakazopatikana zinaelekezwa katika maeneo yenye uhitaji.

Sambamba na hatua hizo, wadau wamehimizwa kushiriki katika kampeni za elimu kwa umma kupitia redio, televisheni na njia nyingine za mawasiliano ili kuongeza uelewa wa wakulima kuhusu malipo, uhifadhi wa mazao na hatua za kujikinga na athari za mvua.

Kikao hicho kimeendelea kudhihirisha umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, vyama vya ushirika, taasisi za fedha na sekta binafsi katika kutambua changamoto, kusikilizana, kufuatilia utendaji na kutekeleza hatua zinazokubaliwa.

Mafanikio ya msimu wa korosho hayapimwi kwa bei nzuri pekee. Yanajumuisha pia ubora wa mazao, usalama wa korosho katika hatua za ukusanyaji na uhifadhi, malipo kwa wakati na uwajibikaji wa kila mdau.
Likes